Kutana na mgonjwa wa UKIMWI aliyepona ugonjwa huo baada ya kuishi nao kwa miaka 31

Wakati suala la Mmarekani kupona virusi vya Ukimwi (VVU) ama HIV ilipotangazwa Julai 2022, habari hiyo ilisifik duniani kote kama hatua nyingine ya kihistoria katika kutafuta tiba ya virusi vinavyosababisha UKIMWI.



Mgonjwa huyu ni mmoja wa watu watano tu duniani ambao wameingia katika kundi la watu waliopona VVU na saratani ya damu (Leukemia) baada ya kufanyiwa upandikizaji wa seli (stem cell transplant).


Akiwa na umri wa miaka 66 na kugundulika kuwa na UKIMWI mwaka 1988, kiumri alikuwa mkubwa zaidi kati ya wagonjwa hao watano, na ndiye aliyekuwa akiishi na virusi hivyo vya Ukimwi kwa muda mrefu zaidi.


Hata hivyo, wakati wa tangazo hilo, alitaka kuhifadhiwa utambulisho wake na hivyo jina lake halikutajwa.


Karibu mwaka mmoja baadae, Paul Edmonds ameamua kujitokeza na hatimaye kusimulia simulizi yake, katika mahojiano yake ya kwanza na chombo cha habari cha Amerika Kusini, alipozungumza na BBC News Brazil.

Edmonds alifanyiwa upandikizajimwaka 2019 katika hospitali ya saratani ya the City of Hope Cancer Center huko California.

"Sikuwa tayari (kuzungumza) kwa wakati huo. Hizi zilikuwa habari njema kwangu, na nilihitaji muda wa kufikiria nilichotaka kufanya," Edmonds aliambia BBC News Brazil.


VVU, kifupi cha Virusi vya Ukimwi hushambulia mfumo wa kinga wa binadamu.


Katika hali yake ya juu zaidi, virusi vinaweza kusababisha UKIMWI, ambayo ni ambao ni Upungufu wa Kinga Mwilini, na kutengeneza njia ya kushambuliwa mfululizo na magonjwa nyemelezi ambayo hutamba kwa sababu ya kushindwa kwa kinga ya mgonjwa.


Katika miaka ya 1980, Edmonds alipogunduliwa kuwa ana VVU, hakukua na chaguzi nyingi za matibabu ya VVU na wengi waliona ukipata VVU hukumu yake ni kifo.


Kwa upande wake, ubashiri ulikuwa mbaya zaidi, kwa kuwa matokeo yalionyesha kuwa, pamoja na kuwa alikuwa na virusi hivi, alikuwa tayari ameshaambukizwa UKIMWI. Vimeshaingia na kushambulia kinga na kumsababishia UKIMWI.


Katika miongo ya hivi karibuni, matibabu mapya yamefanikiwa na leo watu wenye virusi hivi wanaweza kuishi muda mrefu na maisha yenye afya, na wengi hawana hata UKIMWI. Lakini bado hakuna tiba, na watu wanaopatikana na VVU wanapaswa kuishi na virusi na kutumia dawa (ARV) kwa maisha yao yote.


Mafanikio ya suala la Edmonds, iliyoelezewa naye anasema ni kama "muujiza", na yalikuja baada ya utambuzi wa pili.


Mnamo mwaka wa 2018, wakati wa vipimo vya kawaida vya kufuatilia VVU, aligundua kuwa alikuwa na saratani ya damu (Leukemia), aina ya saratani ambayo huathiri bone marrow au uboho na seli za damu.


Edmonds alifanyiwa upandikizaji huo mnamo 2019 katika Kituo cha Saratani cha City of Hope huko California.


Miaka miwili baadaye, mnamo 2021, aliachana na dawa zake za VVU na, hadi leo, yuko katika hali ya utulivu wa muda mrefu, na hana VVU au Saratani inayoonekana katika mfumo wake.

Edmonds na mumewe, Arnie House (kulia), wamekuwa pamoja kwa miaka 31, walifunga ndoa mwaka 2014.


Ingawa aina hii ya upandikizaji ni nadra kwa wagonjwa walio na VVU, madaktari na watafiti wanaona matokeo ya Edmonds na wagonjwa wengine wanne ambao walipona kwa kufanyiwa zoezi hilo ni ishara inayotia moyo.

Wengi wanatumai kuwa ufuatiliaji wa wagonjwa hawa na uchunguzi wa visa hivi unaweza kusaidia kupatikana kwa matibabu mapya na tiba stahiki ya VVU.

" Upandikizaji (A stem cell transplant) ni zoezi tata, lenye madhara makubwa (side effects)," Dk. Jana Dickter, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza na sehemu ya timu inayomtibu Edmonds katika City of Hope, aliambia BBC News Brazil.

"Kwa hiyo si njia sahihi kwa watu wengi wanaoishi na VVU. Lakini ni njia nzuri kwa watu wenye VVU ambao wana saratani ya damu na ambao wanaweza kufaidika na upandikizaji huu kutibu ugonjwa huo," Dickter anasema. .

Kuishi na UKIMWI
Edmonds alikulia huko Toccoa, mji wa watu wasiozidi 10,000 katika maeneo ya vijijini ya Georgia. Licha ya kuishi katika jumuiya ndogo ya kidini na kihafidhina huko Amerika Kusini, wazazi wake walimuunga mkono alipojitokeza na kujitangaza kwamba anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Mnamo 1976, akiwa na umri wa miaka 21, alihamia San Francisco, jiji la California ambalo tayari lilikuwa likijionyesha kama kitovu cha harakati za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

"Mwanzoni, ilikuwa jambo la kushangaza. Ulikuwa wakati wa kipekee sana. Wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja kutoka kila mahali walikuja San Francisco," anakumbuka Edmonds.

Lakini katika miaka ya mapema ya 1980, wengi walianza kuugua. "Ilikuwa hali ya kutisha, hakuna aliyejua kinachoendelea. Waliuita (ugonjwa mpya) saratani ya wapenzi wa jinsia moja. Watu walikuwa na hofu," anaripoti.

Wengi wa wagonjwa wa VVU walikufa ndani ya miaka michache baada ya kugundua kuwa walikuwa na virusi. Edmonds anakumbuka akisoma kumbukumbu za maiti katika moja ya magazeti ya eneo kwenye baa aliyotembelea mara kwa mara, mara nyingi akilia alipoona majina ya marafiki na watu aliowajua.
Wakati Edmonds (pichani na mumewe House) alipodungulika na HIV ama VVU mwaka 1988, hakukuwa na tiba za kusaidia zaidi ya kuonekana ni uhonjwa wa kifo.
Edmonds anasema hakuwa na dalili zozote alipoamua kwenda kupima VVU mwaka 1988, lakini tayari alikuwa na wasiwasi kwamba anaweza kuwa ana virusi hivyo. Anasema haikuwa rahisi kupokea matokeo.

"Bado nakumbuka sura yake, ilikuwa ngumu kwake kunipa habari pia, niliweza kuona hilo usoni mwake," anasema Edmonds, ambaye alikuwa na umri wa miaka 33 wakati huo.

"Nilipimwa na kugundulika nimeambukizwa VVU na pia nilipimwa UKIMWI, kwa sababu hesabu yangu ya T-lymphocyte (CD4) ilikuwa chini ya 200 (kwa kila milimita ya ujazo ya damu), ambayo inachukuliwa kuwa ni UKIMWI," anasema Edmonds. "Ingawa tayari nilishuku kwamba ninaweza kuwa na VVU, kupokea matokeo ilikuwa jambo la mshtuko, (nilishtuka)."

Mwaka 1992, Edmonds alikutana na mume wake, Arnold House, anayemuita Arnie. Edmonds mara moja alimueleza kwamba alikuwa na VVU na akamhimiza pia mumewe House kwenda kupima.

"Alipimwa na kugundulika na yeye ana VVU. Ilikuwa mshtuko, lakini alikabiliana vyema na hali hiyo na maisha yakaendelea," Edmonds anasema, akibainisha kuwa daima wamekuwa pamoja kwa miaka mingi ya kuishi na VVU.

Edmonds anamzungumzia mpenzi wake huyo ambaye ameishi naye kwa miaka 31 na ambaye alifunga naye ndoa kihalali mwaka 2014 akisema : "Hatujatengana tangu siku ya kwanza tulipokutana."

Upandikizaji
Baada ya muda, matibabu mapya na bora zaidi ya VVU yaligunduliwa na wanandoa kuzoea kuishi na virusi. "Unaanza kukubaliana na hali na kufikiria siku zijazo," anasema Edmonds.

Ilikuwa hivyo hadi, mnamo 2018, miongo mitatu baada ya kugundulika ana VVU, Edmonds aligundua kuwa alikuwa na ugonjwa wa myelodysplastic (MDS), neno ambalo linamaanisha kundi la magonjwa yanayoathiri Bone marrow au uboho, tishu za rojorojo zilizo ndani ya mifupa inayohusika na utengenezaji wa seli za damu. Ugonjwa wa Myelodysplastic wakati mwingine huendelea hadi kusababisha saratani ya damu (Leukemia).

Anadai hakuwa na dalili, zaidi ya uchovu kidogo tu. Madaktari wake walimwambia atafute matibabu City of Hope, na hapo wahudumu wa afya walieleza maelezo ya utaratibu huo, kwamba ingekuwa nafasi yake kuishinda saratani na, pengine, VVU pia kama angefanyiwa upandikizwaji huo.




Mnamo Februari 2019, akiwa na umri wa miaka 63, hatimaye alikuwa tayari kwa upandikizaji, ambao ulifanikiwa.

Na katika miezi kadhaa iliyofuata, aliendelea kufuatiliwa kwa karibu na madaktari, huku akisema kwamba alitembelewa na marafiki kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Hakujua kuhusu kupona VVU hali ilipofika Machi 2021, zaidi ya miaka miwili baada ya upandikizaji , ambapo Edmonds hatimaye aliacha matibabu ya kurefusha maisha.

Tangu wakati huo ameondokana na saratani ya damu na VVU, lakini madaktari wanaohusika na matibabu yake bado hawatumii neno "tiba" kuelezea suala hilo.

Kwa mujibu wa Dk. Jana Dickter, kati ya wagonjwa 15 wa VVU duniani kote ambao wamepokea upandikizaji wa aina hii, wanane wamefariki na watano, akiwemo Edmonds, wamepata nafuu ya muda mrefu. Wengine wawili wanaendelea kupokea tiba ya kurefusha maisha.

Ni tiba adimu ambayo haimfai kila mgonjwa, lakini inayotoa matumaini.

#VVU/UKIMWI #AFYA#MUTRAMASTORY255



Comments